HESLB YAFUNGUA DIRISHA LA RUFAA KWA SIKU SABA
Kuwa wazi kwa siku saba (07) hadi Novemba 20
Wanafunzi 68,422 wa mwaka wa kwanza wapangiwa mikopo hadi sasa
Jumapili, Novemba 13, 2022
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo (Jumapili, Novemba 13, 2022) imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la rufaa ili kutoa fursa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba (07) kuanzia leo, Novemba 13 hadi 20 mwaka huu na kuwa rufaa kutoka kwa wanafunzi zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao.
“Hadi leo (Novemba 13, 2022), tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.
HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imetolewa na serikali kutoka mwaka 1994/1995.
0 Comments